#MiakaMiwiliYaMama: Ziara ya Kamala Harris nchini na fursa za kiuchumi kwa Tanzania

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris akianza ziara yake ya siku tatu (Machi 29-31) nchini leo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa na uchumi wameeleza kuwa ujio wake ni matokeo ya kazi kubwa ya kuimarisha diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kimataifa iliyofanywa katika miaka miwili ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa Tanzania, ziara hiyo inalenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha ushirikiano hususani kwenye maeneo ya kimkakati ambayo yanagusa maisha ya Watanzania ikiwa ni pamoja na biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji wa mazingira.

Ziara hiyo imekuja takribani mwaka mmoja tangu Rais Samia alipofanya ziara nchini Marekani, ambapo alimwalika Kamala kuzuru Tanzania, hivyo kuitikia wito huo kunadhihirisha uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Marekani ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 62.

Marekani ni moja ya washirika wakubwa wa maendeleo nchini ambapo imewekeza kwenye miradi 266 yenye thamani ya takribani trilioni 11 ambayo imetengeneza ajira zipatazo 54,584 kwa Watanzania.

Itakumbukwa pia katika ziara ya Rais Samia nchini Marekani Aprili 2022 alifanikiwa kuvutia uwekezaji wa zaidi ya TZS trilioni 2, hivyo ujio wa kiongozi huyo wa juu wa Marekani unatazamiwa kuwa na matokeo zaidi ya hayo katika sekta ya biashara na uwekezaji.

Ni dhahiri kuwa Tanzania kuchaguliwa miongoni mwa nchi zaidi ya 50 za Afrika ni fursa muhimu ambayo inathibitisha kuimarika kwa mazingira ya kisiasa na kiuchumi, na hivyo ziara hiyo itaitangaza zaidi Tanzania kimataifa na kuvutia uwekezaji kutoka Marekani na sehemu nyingine.