Miaka Miwili: Mheshimiwa Rais alivyoiimarisha sekta ya sanaa na kuzalisha ajira kwa vijana

Machi 2023 Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anatimiza miaka miwili tangu achukue usukani wa kuiongoza Tanzania. Watanzania wakitazama nyuma wanaona kuwa amefanya mambo mengi makubwa, ambayo yameboresha taswira ya nchi kikanda na kimataifa pamoja na kuchochea maendeleo ya Mtanzania mmoja mmoja.

Sekta ya sanaa haikuwa mbali kufikiwa na mafanikio haya, ambapo kwa sasa wasanii wana mengi ya kuelekeza kwa namna walivyoshikwa mkono. Haya ni baadhi ya mengi aliyoyafanya;

Kuwa Mwigizaji namba moja wa filamu
Filamu ya kutangaza utalii nchini, Tanzania: The Royal Tour ilikuwa ishara ya kwanza kwa wasanii juu ya namna Rais anavyoitazama kwa umuhimu tasnia ya filamu, na hivyo kuwapa hamasa kubwa wasanii.

Tuzo za Muziki
Machi 2022 tuzo za muziki zilirejeshwa nchini ikiwa ni miaka sita tangu mara ya mwisho zilipotolewa na sasa zinasimamiwa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia. Kurejeshwa kwa tuzo hizo kumewapa hamasa wasanii kufanya kazi bora zaidi za sanaa na kuonesha kuwa Serikali inatambua jitihada zao.

Tuzo za Filamu
Tangu Rais Samia aingie madarakani, tuzo za filamu zimetolewa mara mbili, utaratibu ambao awali haukuwepo, huku Watanzania wakiziona katika nchi nyingine.

Mwaka 2021 tuzo zilitolewa jijini Mbeya na mwaka 2022 zilitolewa jijini Arusha, na hivyo kuongeza motisha kwa wasanii kufanya kazi bora kuanzia uandaaji, picha na maudhui.

Mirabaha
Ombi la miaka mingi la wasanii lilipata majibu ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia ambapo walilipwa fedha kutokana na kazi zao kutumika katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana ambapo TZS milioni 312 zilitolewa.

Mikopo kwa Wasanii
TZS bilioni 2.5 zilizotengwa kwa ajili ya wasanii kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa zinawawezesha wasanii kuboresha kazi zao na kutoa fursa za ajira kwa vijana zaidi.

Rais Samia alifufua mfuko huo ambao uliacha kufanya kazi tangu mwaka 2013, na tayari wasanii wamepewa mikopo ya hadi TZS milioni 40.

Tanzania Mwenyeji mashindano ya kimataifa
Mashindano ya urembo na Utanashati kwa viziwi Afrika yalifanyika nchini Agosti 2021 na kuifungulia Tanzania njia ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ngazi ya dunia. Mashindano hayo yalifanyika nchini Oktoba 2022 na kuendelea kuitangaza nchi na sekta ya urembo na utanashati.

Uteuzi
Sekta ya sanaa na burudani ilipata furaha baada ya mwenzao, Hamis Mwinjuma kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Uteuzi huo umeongeza imani ya wasanii na umedhihirisha kuwa Rais Samia anataka kuona sekta hiyo ikikua zaidi kwa kuteua mtu anayeifahamu anayeweza kuchochea maendeleo yake.

Yote haya yaliyofanyika yamewanufaisha watu mbalimbali kwa kuzalisha ajira zaidi, kuwawezesha wasanii kunufaika na kazi zao za sanaa pamoja na kutangaza nchi kikanda na kimataifa.