Miaka miwili ya Mheshimiwa Rais inavyonufaisha vijana na wanawake kwa mitaji

Msemo wa Wahenga kuwa Mgaagaa na upwa hali wali mkavu umejirihirisha kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na manufaa lukuki yanayowafaidisha Watanzania kutokana na safari za nje ya nchi ambapo manufaa hayo awamu hii yanagusa zaidi wanawake na vijana.

Ziara zake zimewezesha wafanyabiashara kutoka Ulaya kuja nchini wiki iliyopita ambapo kupitia Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) walitoa mikopo yenye masharti nafuu ya TZS trilioni 1.4 kwenye benki za CRDB, NBC na KCB ambayo itawanufaisha wajasiriamali, pamoja na TZS bilioni 318 kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujasiriamali ya Uholanzi (FMO) na Taasisi ya Ufaransa ya Kufadhili Maendeleo (PROPARCO).

Nusu ya fedha za EIB, TZS bilioni 700 zitatumika kukuza biashara za wajasiriamali ambapo TZS bilioni 421 zitaelekezwa kufanikisha miradi na biashara zinazoendeshwa na kusimamiwa na wanawake na TZS bilioni 248 zitatumika kwenye miradi iliyopo kwenye uchumi wa bahari.

Kupitia mikopo hiyo, benki za ndani zitakuwa na uwezo wa kutoa mikopo kwa wanawake na wajasiriamali wengi zaidi ambao changamoto ya mitaji imekuwa kubwa kwao.

Tukio hili moja ni ushuhuda namna kila safari ambayo Mheshimiwa Rais anafanya nje ya nchi imeleta fursa zaidi za kibiashara na kuvutia wawekezaji nchini.