Miaka Miwili: Mageuzi (Reforms) ya Mheshimiwa Rais Samia yanavyoimarisha biashara nchini

Ikiwa mageuzi (reforms) ni moja ya nguzo nne (4Rs) za uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ndani ya kipindi kifupi amefanya mageuzi makubwa kwa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, hatua ambayo imefufua biashara na kuvutia uwekezaji ndani na nje ya nchi.

Mageuzi hayo yaliyofanyika, Rais amelenga kuimarisha taasisi na kuhakikisha sera, sheria, na kanuni zinazosimamia biashara na uwekezaji zinatabirika, lakini pia zinachochea uwazi, zinaondoa ukiritimba na changamoto nyingine ambazo zimekuwa zikikwamisha ustawi wa biashara nchini.

Mafanikio makubwa yamepatikana katika mageuzi hayo ambayo ni pamoja na kufuta kodi na tozo zaidi ya 230 ambazo ziliathiri ukuaji wa biashara. Aidha, Tanzania imeimarisha ushirikiano na mataifa mengine katika masuala ya kikodi ambapo tayari imetia saini makubaliano na nchi 10 kuondoa utoaji kodi mara mbili na kuzuia ukwepaji kodi, moja ya nchi hizo ni Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Zaidi ya hapo mageuzi yamefanyika katika kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato ikiwa ni pamoja na kuhakikisha shughuli za ukadiriaji kodi zinafanyika kwa haki, kuhakiksha ritani za kodi zinafanyika kwa wakati, kutumia mifumo ya kodi ya kidijitali ikiwa ni pamoja na dirisha la mtandaoni linalowawezesha wateja kujihudumia na dirisha la pamoja la kielektroniki linalorahisisha ufanyaji wa miamala.

Pia, Serikali imefanya mabadiliko Sheria ya Rufaa za Kodi, Sura ya 408 na kujumuisha njia mbadala ya usuluhishi wa migogoro na hivyo kupunguza mlolongo mrefu katika kushughulikia rufaa za kikodi. Katika muktadha huo huo, Rais Samia amefanikisha upatikanaji wa sheria mpya ya uwekezaji (Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya Mwaka 2022) ambayo imeiondoa Sheria ya Uwekezaji Tanzania ya Mwaka 1997.

Sheria mpya imeweka mazingira bora zaidi ya biashara ikipunguza muda wa kupata leseni kutoka siku 14 za kazi hadi siku 7 za kazi na pia kutoa nafasi usuluhishi wa migogoro kwenye taasisi za kimataifa.

Kutokana na ukweli kuwa mazingira ya biashara yatafanikiwa kukiwa na amani na utulivu, Rais Samia ameendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa haki, utulivu wa kisiasa na upatikanaji wa huduma za kijamii ili Tanzania iendelee kuwa kitovu cha uwekezaji.