Akiendelea kufanya vizuri kwenye mageuzi ya kiuchumi na kisiasa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amegeukia sekta ya haki ambapo leo amezindua Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuimarisha Taasisi za Haki Jinai ili kuhakikisha zinatoa haki kwa wananchi wa wakati na kwa misingi ya kisheria.
Taasisi ambazo zinakwenda kufanyiwa maboresho ni Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Magereza pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.
Wakati wa mapitio tume hiyo itaangalia masuala mbalimbali kwenye taasisi husika ikiwa ni pamoja na mifumo ya utendaji, mafunzo, mifumo ya ajira, matumizi ya TEHAMA, fikra za kiutendaji na mahusiano kati ya taasisi hizo na raia.
Katika maboresho hayo Rais Samia anelenga kukomesha vitendo mbalimbali ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa na wananchi ikiwa ni pamoja na mamlaka husika kuwabambikia kesi, kucheleweshwa kwa upelelezi, msongamano mkubwa wa mahabusu magerezani, kupambana na rushwa pamoja na kuimarisha uwezo wa taasisi hizo katika kulinda na kutetea maslahi ya nchi kwa kuhakikisha ajira zinatolewa kwa mujibu wa sheria na kunakuwepo mafunzo ya mara kwa mara.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema “hakuna kitu kibaya duniani kukichepusha kama haki ya mtu,” na hivyo kama ambavyo hakuna atakaye haki yake ipokonywe, vivyo hivyo anatakiwa kuhakikisha hashiriki katika upokonyaji wa haki ya mwingine.