Faida ya benki za kibiashara nchini imeongezeka kwa TZS bilioni 400 mwaka 2022 na kuvuka ukomo wa shilingi trilioni moja kwa mara ya kwanza katika historia ya sekta ya fedha nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa za benki ambazo zimetoa taarifa zao za fedha hadi Januari 30 mwaka huu, zinaonesha kuwa zaidi ta TZS trilioni 1.164 zilikusanywa kama faida (net profit) ikiwa ni ongezeko kutoka TZS bilioni 740 zilizokusanywa mwaka 2021.
Ongezeko hilo la faida ambalo limeambatana na kupungua kwa mikopo chechefu, kuongezeka kwa kiwango cha fedha kinachowekwa na wateja wa benki pamoja na mikopo kwa wateja kumetokana kuimarika kwa mazingira mazuri ya biashara nchini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Benki hizo zimesema kuwa ongezeko hilo la faida ni ishara kuwa ajenda ya Serikali ya kukuza biashara inafanya vizuri ambayo inatokana na usimamizi mzuri ikiwemo wa kisera ambazo zinatoa nafasi kwa sekta binafsi kukua.
Ukuaji huo unatarajiwa kuwa na matokeo chanya kwa wananchi kwani unaongeza uwezo wa benki kupanua huduma za kifedha kuwafikia wananchi wengi zaidi lakini pia kuongeza kiwango cha mikopo kwenda sekta binafsi ambayo ina mchango mkubwa kwa maendeleo na kuzalisha ajira.