Haki ni moja ya mahitaji ya msingi kwa kila mwananchi. Akitambua umuhimu huo, Julai 2022 Mheshimiwa Rais SamIA Suluhu Hassan alitangaza kuwa ameunda kamati ya watu watano ikiongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Othman Chade ambayo inafanya kazi ya kupitia miundo na utendaji kazi wa taasisi za haki jamii, kuhakikisha kuwa zinawahudumia wananchi kwa uadilifu.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema mapitio hayo ambayo yameanza na Jeshi la Polisi yatafanyika pia katika taasisi nyingine ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, TAKUKURU, Jeshi la Magereza na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya lengo likiwa ni kuleta mabadiliko ya kiutendaji yenye matokeo kwenye vyombo hivyo.
Hii si mara ya kwanza kwa Rais kuweka wazi azma yake ya kusimamia haki nchini, kwani itakumbukwa kwa agizo lake kwa Polisi kuhusu wenye kesi ambazo hazina ushahidi waachiwe lilipelekea kuachiwa kwa takribani wananchi 2,000 ambao kesi zao hazikuwa na ushahidi wa maana.
“Kabla ya kumpeleka mtu ndani hakikisha umefanya kazi yako vizuri. Una ushahidi wa kutosha ndio unakwenda kumsweka,” alisema Rais Samia akizungumza na maafisa wa Jeshi la Polisi na kueleza kuwa mrundikano mkubwa wa mahabusu ni gharama kwa Serikali kwani inalazimika kuwalisha na kuwapatia huduma za afya, lakini pia ni usumbufu kwa familia.
Hatua nyingine kubwa katika masuala ya haki chini ya uongozi wa Rais Samia ni pale mahakama ilipotoa haki kwa wafungwa kupiga kura, baada ya kubatilisha kifungu cha Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambacho kilikuwa kinapingana na katiba.
Aidha, ameendeleza mapambano dhidi ya rushwa akiamini kuwa rushwa inamzuia mwenye haki kupata haki yake na asiyestahili anaipata, akitolea mfano wakati wa uchaguzi ambapo wasio na fedha wanaweza kujikuta hawachaguliwi kwa kushindwa kutoa rushwa.
Wakati huo huo, ameendelea kutekeleza ahadi yake ya maridhiano kwa kukutana na kuzungumza na vyama vya siasa akifahamu kuwa haki haiwezi kustawi sehemu isiyo na amani, lakini pia haki ndio msingi wa Taifa kuwa na amani, umoja, ushirikiano ambavyo kwa pamoja vyote husuma maendeleo ya Taifa mbele.