Tanzania inaendelea kujiimarisha katika mkakati wa kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji pamoja na biashara ambapo leo imesaini mkataba na mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kipande cha sita cha reli ya kisasa kutoka Tabora hadi Kigoma (506km) kwa gharama ya TZS trilioni 5.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Dkt. Samia amesema kuwa “hilo litafanikiwa tukihakikisha miradi yote tunayoitekeleza, tunaisimamia na kuikamilisha kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.”
Ujenzi wa kipande cha Tabora – Kigoma ambacho kitaungana na kipande cha Uvinza-Musongati-Kindu itaiunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DCR), upande wa mashariki ambapo kuna mizigo mingi inayohitaji kusafirishwa kwenda na kutoka Bandari ya Dar es Salaam, ikifahamika kuwa mwaka 2021 taifa hilo lilipitisha mizigo ya tani milioni 2.4 katika bandari hiyo.
Aidha, ujenzi wa reli hiyo utachochea ukuaji wa biashara kwa kupunguza gharama za kusafirisha mizigo kwenda DRC ambapo sasa gharama za kusafirisha kontena moja hufika hadi TZS milioni 35, huku ikichukua hadi mwezi mmoja. Kuanza kutumika kwa reli kutapunguza muda na gharama hadi kufikia TZS milioni 9 na muda wa siku moja, huku ukiwa usafiri ulio salama zaidi.
“Takwimu zinaonesha ujenzi wa reli hii utasaidia kufungua maeneo yenye machimbo ya madini yenye mzigo wa zaidi ya tani milioni 150 na mizigo mingine ya kuwezesha migodi hiyo kufanya kazi,” ameeleza Dkt. Samia.
Mbali na hayo ujenzi wa reli umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania ambapo zaidi ya wananchi 20,000 wamepata ajira za moja kwa moja, huku waajiriwa wakilipwa TZS bilioni 237.7. Pia umetoa zabuni kwa Watanzania zenye thamani ya takribani trilioni 2 na hivyo kuiwezesha Serikali kukusanya kodi TZS bilioni 949.