Baada ya kusubiri kwa zaidi ya miaka tisa, hatimaye Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi ambacho kimewezesha watumishi katika kada mbalimbali kushuhudia kuongezwa kwa mishahara yao.
Mara ya mwisho kutolewa kwa viwango vya kima cha chini kwa sekta binafsi ilikuwa mwaka 2013, na hivyo watumishi wa sekta hiyo walikuwa wakiisihi Serikali kupandisha viwango vya mishahara ili kuweza kumudu gharama za maisha.
Katika viwango ambavyo vitaanza kutumika Januari 2023, mfano, watumishi wa majumbani watalipwa hadi TZS 250,000 kwa mwezi, huku wale wanaofanya katika sekta za huduma ya mawasiliano wakilipwa hadi TZS 500,000.
Mbali na nyongeza hiyo, Serikali imeanisha maslahi mengine ambayo watumishi wa sekta binafsi watastahili ikiwa ni pamoja na likizo ya mwaka yenye malipo, posho itakayotolewa mara moja kwa kila miaka miwili na posho nyingine kama watakavyokubaliana.
Aidha, dereva wa lori atastahili posho kwa ajili ya umbali wa safari, na kwa mtumishi ambaye kwa sasa anapokea mshahara na maslahi bora kuliko yaliyoanishwa na amri mpya ya kima cha chini, ataendelea kupokea mashahara huo huo ikiwa amejiriwa na mwajiriwa huyo huyo.
Kuongezeka kwa viwango hivyo, kwanza ni hatua ya Rais Samia kutimiza ahadi yake ya kuboresha maslahi ya watumishi nchini kwa lengo la kuinua hali zao za kiuchumi ili waweze kumudu gharama za maisha.
Pili, nyongeza hiyo ambayo itawagusa Watanzania wengi ambao wameajiriwa kwenye sekta hiyo itawawezesha kumudu gharama za maisha, ambapo awali ilikuwa changamoto kwao, itachochea ukuaji wa uchumi na kukuza sekta nyingine.