Wanayoyatamani Watanzania kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais Samia nchini China

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini China kuanzia Novemba 2 hadi 4 mwaka huu kufuatia mwaliko wa Rais Xi Jinping suala la uendelezaji wa eneo maalum la kiuchumila Bagamoyo (BSEZ) ni moja ya ajenda atakazozibeba.

Mwaliko huo uliokuja siku chache baada ya Rais huyo wa Taifa kubwa la Asia kuchaguliwa kwa muhula wa tatu kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Watu wa China (CCP) unamfanya Rais Samia kuwa mkuu wa nchi wa kwanza kutoka Afrika kuzuru nchi hiyo.

Kufuatia mwaliko huo unaolenga kukuza ushirikiano baina ya mataifa haya mawili, baadhi ya Watanzania wameeleza matamanio yao ikiwa ni pamoja na China iombwe kukarabati reli ya TAZARA na kujenga daraja juu ya bahari kutoka Dar es Salaam hadi Zanzibar.

“Ni faraja kusikia Rais Samia amepata mwaliko wa Rais Jinping, ningetamani sana pamoja na mambo mengine hili la kuboresha TAZARA na kujenga daraja yame miongoni mwa vitu ambavyo ataviomba,” amesema Profesa Humphrey Moshi.

Kwa upande wake Msemaji Mkuu Serikali, Gerson Msigwa amesema miradi inayofanyika na nchi hizi mbili ni mingi na mingine inakuja na kwamba na kwamba itakapokamilika Watanzania watajulishwa.

Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) hadi January 2021 kwa upande wa Tanzania Bara China ilikuwa ina jumla ya miradi 940 iliyozalisha ajira takribani 120,000.