Benki ya Dunia (WB) imeipongeza Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi hali inayoonekana kama miujiza wakati huu ambapo chumi za nchi mbalimbali duniani zinadorora kutokana na athari za janga la UVIKO19, vita ya Urusi na Ukraine, kupanda kwa bei ya mafuta na mabadiliko ya tabianchi.
Akitoa pongezi hizo, Makamu Rais wa Benki ya Dunia wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Victoria Kwaka amesema kuwa wakati nchi mbalimbali zikihangaika na janga la mfumuko wa bei wa tarakimu mbili, huku akiitaja Ghana kuwa na mfumuko wa bei wa 30%, Tanzania imeweza kuwa na mfumuko wa bei wa tarakimu moja tu, ambapo kwa Septemba ulikuwa 4.8%.
Athari za kuwa na mfumuko mkubwa wa bei ni kuwa kunapandisha bei za bidhaa, kunapunguza uwezo wa kufanya manunuzi, hivyo kuathiri hali ya maisha ya wananchi.
“Tumeona karibu nchi nyingi duniani zikiwa na akiba ndogo ya fedha za kigeni, lakini Tanzania imeweza kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi mitano,” amesema Kwaka.
Fedha za kigeni zinaiwezesha serikali kutimiza mahitaji yake ya fedha za kigeni na mahitaji ya kuagiza bidhaa kutoka nje, kutoa imani kwamba serikali inaweza ikatimiza majukumu yake ya muda mfupi kulipa madeni ya nje na kusaidia utekelezaji wa sera za fedha na kubadilisha fedha za kigeni, pamoja na uwezo wa kuingilia kuhakikisha fedha ya taifa ni imara.
Kuhusu nakisi ya bajeti amesema mataifa mataifa mengi yakihangaika kwa kuwa na nakisi kubwa ya bajeti, Tanzania ina nakisi ndogo ya 3.5% ya Pato la Taifa.
Nakisi ndogo ya bajeti kwanza ni ishara nzuri kuwa uchumi wa Taifa unaimarika na ina maana kuwa nchi itahitaji kukopa kiasi kidogo cha fedha au kutokuweka kodi kubwa ili kupata fedha za kufadhili bajeti yake.
Kwaka pia ameipongeza Tanzania kwa kuwa na sera nzuri za fedha na uchumi zinazoleta utulivu kwenye uchumi na usimamizi bora wa uchumi, hivyo kuiwezesha nchi kutekeleza miradi inayoboresha maisha ya Watanzania.
“Ni matarajio yetu kuwa tutaitumia Tanzania kama mfano bora wa kuigwa na nchi nyingine duniani,” alihitimisha Kwaka.