Mauzo ya Tanzania nchini Kenya mwaka 2021 yalikua kwa asilimia 42 kutoka TZS bilioni 537 mwaka 2020 hadi TZS bilioni 929 mwaka 2021, mchango mkubwa ukitokana na kutatuliwa kwa vikwazo vya kibiashara.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika kipindi tajwa, Tanzania ilishuhudia ongezeko la usafirishaji wa chai, mahindi, ngano, alizeti, mchele, maharagwe, mbogamboga, karatasi, bidhaa za chuma, marumaru, saruji, vioo na bidhaa za vioo, sabuni na vipodozi kwenda Kenya.
Akizungumza leo wakati wa ziara ya Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto nchini Tanzania, Rais Samia Suluhu amesema kwamba wataalamu wa pande zote walibaini uwepo wa vikwazo 68 visivyo vya kikodi, ambapo vikwazo 54 vimetatuliwa na 14 bado havijatatuliwa ambapo wametumia jukwaa kueleza kuwa wamedhamiria kutatua vikwazo vilivyobaki, ili wananchi wa pande zote ambao wana uhusiano wa kindugu, kihistoria na kijiografia wanafanya biashara kwa uhuru kwani kukua kwa biashara kunanufaisha pande zote.
“Tumekubaliana ya kwamba mawaziri wakutane, maafisa wengine wakutane, tuyakamilishe, tuyaondoe ili biashara iweze kukua zaidi kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Kenya tukiwa sote ni watu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Rais Ruto.
Aidha, amesema “wakati wewe [Rais Samia] na Rais Uhuru Kenyatta mlipokuwa mnafanyia kazi vikwazo hivi, watu walidhani Kenya itanufaika zaidi kuliko Tanzania, lakini Tanzania imenufaika zaidi Kenya.
Kwa kuangazia takwimu za biashara, Kenya ni mshirika mkubwa wa kibiashara na utalii kwa Tanzania, na hiyo huenda imechangia Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki ambayo Rais Ruto amefanya ziara ya kikazi tangu alipoapishwa Septemba 13 mwaka huu.