Jumla ya wanafunzi 1,384,340 wamefanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na mwaka 2021. Wanafunzi wao ni zao la kwanza mpango wa elimu bila ada ulioanza mwaka 2016, ulioshuhudia idadi kubwa ya watoto wakiandikishwa darasa la kwanza.
Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha TZS bilioni 160 ambazo zitatumika kujenga madarasa 8,000 kwenye shule za sekondari 2,439 zilizoainishwa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa nchini.
Madarasa hayo yatakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi 400,000 ambao ni sehemu ya wanafunzi 1,148,512 wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023. Idadi ya wanafunzi wanaobaki watatumia vyumba vya madarasa vilivyoachwa na wanafunzi 422,403 waliohitimu kidato cha nne mwaka huu, pamoja na madarasa katika shule mpya za kata 231 zilizojengwa.
Katika salamu za heri kwa watahiniwa hao Rais amewaahidi kuwa “Serikali itahakikisha maandalizi ya miundombinu ya kuwapokea wote watakaoendelea na kidato cha kwanza mwakani 2023 inakamilika.”
Mwaka 2021 aliweka historia kwa kuwezesha wanafunzi wote waliofaulu kidato cha kwanza kuanza masomo kwa wakati mmoja baada ya kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000, hivyo kuweka mazingira rafiki ya ufundishaji na watoto wote kupata muda sawa masomo.
Kwa hatua hii, Rais Samia anatekeleza matakwa ya ibara ya 11(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoitaka Serikali kufanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa na za kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote za shule na vyuo vinginevyo vya mafunzo.